Vijana tumieni wazee kupata maarifa-Ask Msonganzila.

April 14, 2019
.Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewataka vijana kuheshimu wazee kiumri na hata kimadaraka ili waweze kupata kujifunza mambo mengi yenye hekima na busara kutoka kwao,na hivyo kuwa wazee bora wa baadae katika familia zao.

Askofu Msonganzila ameyasema hayo wakati wa Misa Takatifu ya Jumapili ya matawi ambayo kikanisa inajulikana kama jumapili ya vijana, iliyofanyika katika Kanisa kuu Jimboni humo,na kuhudhuliwa na vijana kutoka katika kila parokia.

“wasikilizeni wazee ,mnaweza kuwa na papala kulingana na damu zenu kuchemka ,lakini tusiwadharau ,tuwape nafasi wanalao jambo la busara la kutusaidia sisi ,na hata ninyi mnakoelekea ni kwenye uzee wa madaraka na umri ,hivyo tuwatumie katika kupata mang’amuzi ya mambo mbalimbali kwa kuwa wameona mengi”amesema Askofu Msonganzila.

Askofu huyo amewataka vijana kujiepusha na maandamano yenye viashiria vya uvunjivu wa Amani huku akiwaasa kufanya maandamano ya kumtukuza Kristo, kwani matawi waliyoyabeba yawe ishara ya kuteseka na Kristo na kisha kufufuka naye.

Amewatakumbusha pia kuwa wavumilivu katika maisha kama ambavyo Yesu Kristo alivumilia mateso yote pale msalabani japokuwa alikuwa anafahamu kuwa anakwenda kufa na wala hakukimbia ,kama ambavyo vijana wengi wakikumbana na changamoto za maisha wanakimbia sehemu zingine kutafuta maisha .

“kokote unakoenda hakikisha unapeprusha bendera ya Yesu ,bebeni Sura yake iwe kimaongezi ,kimahusiano na hata katika kutetea na kuliendeleza kanisa ,kwani kanisa linawekeza sana kwenu vijana,kwa sababu ndio nguvu kazi imara ya umisionari ,msijiamini sana jifunzeni kuwa wapole ,kwa kuheshimu siri na zawadi ya uhai kwani wengi tunatuhumiwa sana kwa kutodhamini dhamani ya uhai,msikatishe maisha ya mtu mwachieni Mungu”ameongeza.

Aidha amewaasa kuhakikisha wanapojenga nyumba zao za kuishi wanakuwa na chumba maalum kwa ajili ya kusali na familia zao,ili kujenga familia inayomtukuza Mungu kila wakati ,pasipo kusubiri hadi waje kumtukuza Mungu Kanisani,kwa kuwa sala ndio msingi wa familia bora katika jamii.

Amewataka pia kuhakikisha wanajiepusha na aina mbalimbali za fujo ili waweze kujitenga na kupata nafasi ya kutosha kusali na kuzungumza na Mungu katika kuwasaidia kupambana na changamoto za kidunia.