MAPADRI MSIONE AIBU KUKEMEA MAOVU YANAYOTOKEA KATIKA JAMII-ASK.MSONGANZILA

12/08/2021

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewataka mapadri kutoona aibu wala kutoogopa kukemea mabaya yanayotokea katika Jamii,kutetea haki,na kutafuta amani ya kweli, bali wawe jasiri katika kuyashinda yote kwa kuwa hiyo ndio gharama ya kuitwa mfuasi wa Kristo.

Hayo ameyasema wakati wa Misa ya kutoa daraja Takatifu la Upadri kwa Padri Phillip Makondo wa shirika la Ufufuko ,iliyofanyika katika Parokia ya Butiama Jimbo Katoliki la Musoma Agosti 12 ,2021,ambaye ni padre wa kwanza Mwafrika katika shirika hilo tangu lianze Utume wake Katika nchi za Afrika na hasa katika nchi ya Tanzania na zaidi ndani ya Jimbo Katoliki la Musoma mwaka 2002 .

“Endeleeni kuhubiri vizuri ,msione aibu kuteseka kwa ajili ya kutetea amani na umoja maana tayari Neno la Mungu limegusa midogo yenu mkiweza kuyafanya hayo ndio itakuwa gharama ya kuitwa na Mungu , nanyi mkaitika kuwa nipo hapa nitume mimi ”Amesema Askofu Msonganzila.

Paroko wa Parokia ya Butiama Padri Daniel Inc ametoa wito kwa wazazi na walezi kutoa vijana wao kujiunga na shirika la Ufufuko kwani malezi yake hayatofautiani na malezi ya mashirika mengine,zaidi anaomba vijana wajitoe kwa wingi ili kuongeza ng’ombe wengi katika zizi la Bwana.

Akitoa neno la shukurani kwa wazazi wa Padri Philip,Padri Inc amesema wameonyesha moyo wa upendo kwa kuwaamini na kutoa sadaka ya kijana wao ili aende kumtumikia Mungu,na kwamba kama shirika wataendelea kuwa pamoja katika sala ili Mwenyezi Mungu akamilishe kazi yake aliyoipanga.

Amewashukuru wote waliofika katika sherehe za kutolewa kwa daraja la Upadri pamoja na michango yao ya hali na mali katika kufanikisha shughuli hiyo,hasa kwa mkuu wa shirika hilo,Recta wa seminari ndogo na mkuu wa nyumba yao ambaye ni Paroko wa Parokia ya Buhemba Padri Marthias Braun pamoja na waamini wote.

Akitoa salam za Serikali Mkuu wa Wilaya ya Butiama Moses Kaegele amempongeza Padri mpya kwa kufikia hatua ya kupewa daraja Takatifu la Upadri kwani kuna mengi amepitia lakini aliyavumilia,hivyo asiache kumwomba Mungu ili aendelee kumsaidia katika Utume wake.

Mkuu huyo pia amewaomba wananchi wa Wilaya hiyo, kuendelea kuchukua tahadhali ya maambukizi ya ugonjwa kwa Uviko-19 ikiwemo kupata chanjo lakini pia kuvaa,barako,kutumia vipukusi na kukaa umbali wa mita moja ili kuendelea kulinda afya zao.