MAKATEKISTA WAPONGEZWA NA ASKOFU MSONGANZILA


Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewapongeza Makatekista wa Parokia ya Iramba Jimboni humo kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya ya uinjilishaji kiroho, ambapo zaidi ya waamini 1149 wamepokea Sakramenti ya Kipaimara kwa mara moja.

Pongezi hizo amezitoa wakati wa Homilia Takatifu Agosti 14,2022 wakati wa ziara yake ya Kichungaji katika Parokia hiyo,na kusema bila juhudi za Makateksta kuwafikia waamini hao na kuwaimarisha kiroho wasinge pata idadi kubwa ya waamini hao.

“Makatekista mna fanya kazi nzuri sana,hii inaonyesha ni kwa namna gani Kanisa linatoa mafundisho yanayolenga kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi yake ya asili na kumjua Mungu ,kumpenda na kisha kumtumikia ili mwisho wake tupate kufika kwake,idadi hii ya waamini 1149 ni kubwa na mnastahili pongezi” amesema Askofu Msonganzila.

Amewaomba waamini waliopokea Sakramenti hiyo kuhakikisha wanaendelea kumtukuza Mungu kwa kufanya yale yanayompendaza Mungu ili kuwa chachu na kielelezo kizuri kwa wengine na hata kuwa mfano wa kuigwa katika jamii ,kwa kufanya matendo mema.

Paroko wa Parokia hiyo Padri Samson Awach, amewashukuru makatekista pamoja na waamini wote wa parokia hiyo kwa kuendelea kuwa imara kiroho hasa katika kulitangaza neno la Mungu hata kwa wale wasioamini ikiwa ni pamoja na kufanya matendo ya Huruma ndani na nje ya kanisa.