WAAMINI KUWENI WANYENYEKEVU-ASK MSONGANZILA.


Waamini nchini wamekumbushwa wajibu wa kuwa wanyeyekevu sio tu kwa muonekano wao bali pia kwa matendo yao ili kuweza kufikia Utukufu wa Mungu,na hivyo jamii inayowazunguka kuiga mfano bora kutoka kwao.

Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila wakati wa Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 105, kubariki nyumba ya mapadri na kisha kupanda miti katika Parokia teule ya Bikira Maria wa Fatima – Songe, jimboni humo.

“ Naomba niwakumbushe waamini wenzangu tuwe wanyenyekevu mbele za Mungu kwa maneno na vitendo,sasa hivi watu unyenyekevu umeisha miongoni mwetu,watu wanauana hovyo hawaogopi,wanafanya matendo ambayo hayaonyeshi utukufu mbele za Mungu nay eye anajiita mkristo,tuachane na tabia chafu Mungu alikuwa mnyeyekevu mtii na hata mauti na ndio maana alikufa kwa ajili ya dhambi zetu”amesema Askofu Msonganzila.

Askofu huyo amesema amewaasa walipata kipaimara kuwa mfano mzuri wa kuigwa na jamii kwa kuwa watu wengi maadili yameshuka na hawana unyenyekevu hasa wanapokuwa katika mikusanyiko ya watu wengi sehemu ambayo heshima na adabu inatakiwa kuonyeshwa si kwa mkubwa tu bali hata kwa mdogo ili kuonyesha utu na ubinadam.

Msimamizi wa Parokia hiyo Teule na Katibu wa Askofu Padri Alexander Muganyizi amemshukuru Askofu huyo kwa kufika katika Parokia hiyo na kutoa Sakramenti ya Kipaimara ,kubariki nyumba ya mapadri na kisha kupanda miti hali ambayo imewaamsha zaidi waamini wa Parokia hiyo kiimani lakini pia ameonyesha upendo kwa waamini wa Parokia hiyo.

“ Asante Sana baba kwa kukubari kufika na kusali nasi,kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara ,kubariki nyumba ya mapadri na kupanda mti ambao kwetu ni ishara ya upendo na kumbukumbu nzuri uliyoiacha kwa kizazi cha sasa na cha baadae,nasi tunakuahidi kuyatunza mazingira haya ”amesema Padri Muganyizi.

Mwenyekiti wa Parokia teule Frank Mageta amemshukuru baba Askofu kwa kuwa nao pamoja na kutoa sakramenti hiyo,kubariki nyumba na kupanda miti na waamimi kwa ujumla kwa ilikuwa ni kiu ya moyo wao ambapo wamefarijika sana na kuendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema ya roho na mwili.