WAAMINI WAASWA KUBUNI MIRADI


Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewataka mapadri na waamini wa jimbo hilo kubuni miradi ambayo itawasaidia katika kukuza kipato cha Parokia na waamini kwa ujumla.

Hayo ameyasema wakati wa uzinduzi wa ofisi za parokia na vyumba 15 vya maduka katika Parokia ya Nyamwaga Jimboni humo, wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kichungaji Parokiani hapo

“Hali sasa inaendelea kubadilika, wafadhili nao wanapungua kutokana na majanga mbalimbali yanayoikumba dunia,hivyo ni vema sasa tuanze kubuni miradi itakayotusaidia kukuza uchumi wa Parokia lakini pia muumini mmoja mmoja. Niwapongeze sana waamini wa Nyamwaga na Paroko wenu kwa ubunifu huu,hapa sasa patachangamka sana na pato la parokia litakuwa ” amesema Askofu Msonganzila.

Amewaomba mapadri wengine katika Jimbo la Musoma kuiga mfano huu kwani kila Parokia inauwezo wa kufanya hivyo,kwani ipo siku mambo ya kuomba omba huko nje yataisha na wafadhili wengi sasa wameanza kupungua.