MCHANGO WA PADRI MAKORI NCHINI MAREKANI WAONEKANA-TEC YATOA NENO.


Baraza la maaskofu Tanzania limempongeza Padri Raphael Makori wa Parokia ya Iramba Jimbo Katoliki la Musoma, kwa moyo wake wa ukarimu anaouonyesha kwa viongozi wa kanisa hasa wanapokwenda nchini Marekani kwa shughuli mbalimbali za maendeleo ya Kanisa hususani kanisa la Tanzania

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padri Charles Kitima, wakati wa sherehe ya miaka 25 ya Jubilei ya Padri Makori iliyofanyika katika Parokia ya Iramba Jimbo Katoliki la Musoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Parokia hiyo.

“Tunakushukuru sana kwa Utume wako Padri Makori, nchini Marekani, kwa namna unavyowakarimu na unavyowaandalia mazingira mazuri Maaskofu wetu wanapokuwa huko Marekani kwa shughuli za Kikanisa,kweli huwa wanajisikia wako nyumbani Tanzania,wanakuombea uendelee na moyo huo huo wa ukarimu ” Amesema Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padri Kitima.

Padri kitima amesema, Utume wake nchini Marekani umekuwa na mafanikio makubwa si kwa Jimbo Katoliki la Musoma tu bali hata katika Majimbo mengine ya nchini Tanzania,kwani anapohitajika kutoa msaada wa jambo fulani analifanya kwa ukamilifu.

Akitoa neno la shukrani kwa wote waliofika katika sherehe yake ya Jubilei ya miaka 25 ya upadri, Padri Raphael Makori amemshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, amewashukuru wazazi,ndugu jamaa na marafiki waliomuombea mpaka yeye kuyatimiza yote hayo.

pia amemshukuru sana Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila,kwa kumtuma masomoni nchini Marekani,na baadae kumuomba abakie huko kwa niaba ya Jimbo la Musoma,ambapo amesema hakika analiwakilisha vema Jimbo la Musoma na anafanya kazi bila kujibakiza,kwaajili ya Utukufu wa Mungu.