ACHENI USHIRIKINA NA VITENDO VYA UKATILI KWA WATOTO-ASK MSONGANZILA


Waamimi nchini wamekumbushwa kuachana na tabia ya vitendo vya ukatili na ushirikina vinavyoendelea katika jamii, kwa sababu ya kutaka mali na utajiri wa haraka, hali ambayo inaonyesha ni ukosefu wa amani ndani ya mioyo yao.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amekemea vitendo hivyo wakati wa Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu kwa kuanza mwaka mpya 2023 tukiwa salama, lakini pia siku ya somo wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mungu Kanisa kuu na msimamizi wa Jimbo la Musoma.

“Tumeanza mwaka mpya 2023 naomba kila mmoja wenu aanze maisha upya,vitendo vya ukatili vimezidi ndani ya jamii,ubakaji,ulawiti na hata mauaji ya watoto wasio na hatia na wanaofanya haya ni ndugu wa karibu! Mama, mjomba na baba, harafu hao hao ndio wanakuwa mashahidi wa kwanza mahakamani wa vitendo hivyo, hapana hii haikubaliki acheni kabisa na sheria ichukue mkondo wake ”amekemea Askofu Msonganzila.

Askofu amewakumbusha waamini, kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai tangu mwaka 2022 uanze mpaka 2023, ametabanaisha kuwa ametutendea mengi hata ambayo sio mastahili yetu kwani anatupenda,wengine wamefariki, sisi tulio hai tumshukuru Mungu kwa yote, hatuna cha pekee zaidi ya upendeleo tu,kila mmoja popote alipo anapaswa kusema asante Mungu kwa zawadi ya uhai.

Amesema tunapoanza mwaka lazima tuombe amani duniani kwa moyo wa dhati na kwa kuweka dhamira yenye hofu ya Mungu, maana ukiwa na amani moyoni mwako hutatenda dhambi,utawahurumia wenzako wakiwemo,majirani zako,watoto wa ndugu yako,mtoto wako mwenyewe na hata watu wengine.

Askofu Msonganzila amesema kila mmoja ana nafasi yake katika jamii na Kanisa, bila kuangalia hali uliyonanyo wala mazingira uliyonayo kwani, hata Yesu Kristo alizaliwa sehemu iliyodhaniwa kuwa ni duni na chafu(kwenye hori la ng'ombe), lakini sehemu hiyo ndio patakatifu,hivyo ni wajibu wetu tunapoanza mwaka kila mmoja atimize wajibu wake kwa nafasi yake.

Paroko wa Parokia hiyo Padri Medard Chegere amemshukuru Mhashamu Baba Askofu kwa ujumbe mzito wa mwaka mpya,ambapo amewapongeza waamini kwa kuvuka mwaka salama na kuanza mwaka wingine pia amewashukuru waamini wote kwa majitoleo yao katika kujenga Kanisa la Mungu na Taifa kwa ujumla.

Akitoa salamu za mwaka mpya mwenyekiti wa Halmashauri ya walei Jimbo Dkt Costantine Mniko, amewaomba waamini kuzingatia mafundisho waliyopewa na kuhani mkuu,na zaidi amesisitiza kila mmoja kusherehekea siku ya mwaka mpya kwa kiasi.