ASKOFU MSONGANZILA AWAPONGEZA NYAMONGO KWA UJENZI WA KANISA


Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewapongeza waamini wa Parokia ya Nyamongo Jimboni humo, kwa Majitoleo yao makubwa katika kujenga nyumba ya Mungu na kuwa sehemu ya uinjilishaji kupitia majitoleo yao,na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na waamini wengine.

Pongezi hizo amezitoa Januari 19,mwaka huu wakati wa Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa hilo, baada ya kufanyika ukarabati mkubwa wa Kanisa hilo ambapo zaidi ya shilingi Milioni 600 zimetumika katika kufanya ukarabati huo na maboresho mengine ndani ya Kanisa.

&Idquo; Leo hii tunatabaruku Kanisa lenu nanyi pia tunawatabaruku hata wale wote ambao walikuwa wamekimbia kwa sababu ya michango ya ukarabati huu,hakika ninyi wana Parokia ya Nyamongo mmekuwa watakatifu ,lakini msibweteke kwa kuitwa watakatifu mkavimba kichwa hapana, kazi sasa ya uinjilishaji ndio imeanza ,endeleeni kushikamana hivyo na kuwa wamoja,kwa majitoleo yenu haya makubwa Mungu awabariki pale mlipotoa na awaongezee Zaidi ” Amesema Askofu Msonganzila.

Askofu Msonganzila amewakumbusha waamini hao kuwa katika kushirikiana ,kuvumiliana kunyenyekeana,na kusamehemana kazi ya Mungu imesonga mbele,lakini pia tendo la kutabaruku Kanisa hilo liwape nafasi ya kusameheana hasa pale mlipokoseana katika harakati za kuhakikisha kazi ya Mungu inakamilika kwa wakati na hatimaye kutabarukiwa.

Askofu pia amekea suala la ukeketaji kwa watoto wa kike na kusema kuwa Nyamongo sasa kupitia Kanisa hilo, imani ya kuwakeketa wasichana iondoke na wabaki na imani ya kusali katika magumu yote wanayo pitia kwenye maisha na kumuomba Mungu imani hiyo potofu ya ukatili kwa watoto wa kike iondoke kabisa mioyoni mwao.

Paroko wa Parokia hiyo Padri Edward Fullbert Shayo amemshukuru Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila kwa kukubali kutabaruku Kanisa hilo,lakini pia amewashukuru waamini kwa majitoleo yao makubwa na ya mfano wa kuigwa ambayo kila mmoja alifanya kwa mapenzi yake bila kusukumwa na mtu kwa ajili ya ujenzi wa hekalu la Mungu,bila kutegemea fedha yoyote kutoka kwa wafadhili.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo na mhamasishaji mkubwa wa ujenzi wa Kanisa hilo Nicodemus Keraryo amewashukuru waamini wote wa Parokia ya Nyamongo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nyumba ya Mungu inakuwa nzuri na yenye kuwavutia waamini wengine hata wale waliokuwa wamekimbia na kwenda kwenye makanisa mengine.

Nao waamini wa Parokia hiyo wamesema wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufanikisha ukarabati mkubwa wa Kanisa lao,maana hapo awali kanisa lilikuwa limechoka na hata baadhi ya waamini walihamia katika madhehebu mengine,lakini sasa wote wamerudi na kanisa sasa limekuwa dogo.