ZAIDI YA WANANDOA 100 WAPATA SEMINA YA MALEZI BORA YA FAMILIA KATIKA PAROKIA YA UTEGI


Wanandoa katika Parokia ya Utegi Jimbo Katoliki la Musoma wamekishukuru Chama cha Utume wa familia katika Parokia hiyo, kwa kuandaa semina kwa wanandoa zaidi ya 100, lengo ikiwa kuwakumbusha mambo madogmadogo na ya muhimu katika ndoa, ambayo wengi wao wameyaacha kwa kudhani kuwa hayana umuhimu tena baada ya kuoana.

Wakizungumza mara baada ya kupata semina hiyo ya siku moja kuelekea siku ya wapendanao iliyofanyika Februari 18 ,2023, wanandoa hao wamesema semina hiyo imewaimarisha zaidi katika kuwajenga na kuwakumbusha mambo muhimu ambayo wengi walikuwa wameshaacha kuyafanya kwa wenza wao wakidhani kuwa kuendelea kufanya hivyo ni kujidhalilisha kwa wenza wao.

&Idquo;mimi nina miaka 10 katika ndoa yangu na kuna vitu kama kumtumia meseji za mahaba mke wangu,kumnunulia zawadi ,kutoka naye out na mambo mengine, kwangu nilikuwa nimeacha kabisa ila kupitia semina hii sasa najiona kama ndoa yangu ina mwezi mmoja na hivyo yanipasa kuyaendeleza yale ya mwanzo wa uchumba wetu ”. amesema Emmanuel Odero

Mwenyekiti wa Parokia hiyo Fredy Kyalawa amewashukuru wawezeshaji wa semina hiyo kwani imewaimarisha na kuwakumbusha mambo muhimu katika malezi ya familia,kwa kuwa wengi wao walikuwa wameshajisahau na kuona kuwa hayo mambo madogomadogo sio wajibu wao tena, kumbe ni vitu vinavyofanya ndoa nyingi kuvunjika kutokana na wengi kupuuza mambo hayo .

Mwenyekiti huyo amesisitiza pia wanandoa kuendelea kuwa karibu na Mwenyezi Mungu na kushiriki shughuli mbalimbali za kulijenga Kanisa, maana familia isiyojiweka karibu na Mungu ni rahisi kupata vishawishi na pasipo kutumia hekima na kusali kwa bidii matokeo yake yanakuwa mabaya na hivyo kuacha watoto wakiteseka pasipo msaada.

Paroko wa Parokia hiyo Padri Innocent Mwesigwa amesema utume wa familia ukisimama imara ndani ya kanisa kila jambo litakwenda vizuri, hivyo semina za mara kwa mara kwa wana ndoa ni muhimu sana na kama Parokia wameona matunda mazuri ya semina hizo kwani ndoa nyingi zinafungwa na zinadumu,wanaume wanaelewa sasa maana ya kuwa na mke mmoja na kuachana na mila zao za kuoa wake wengi, mambo ambayo yote ni matokeo ya semina hizo.

Jerome Mmassy mwanautume wa familia, Mwalimu na mwezeshaji kutoka shirika la Msalaba Mtakatifu amesema wanandoa wengi wamekuwa wakiingia kwenye ndoa kama fasheni fulani kitu ambacho ni hatari sana, ambapo amewasihi wanafamilia kuhakikisha wanadumu katika ndoa zao ili kukamilisha agano la mwenyezi Mungu kwani haiwezekani ndoa inafungwa baada ya muda mfupi wanandoa hao wanawahi kuachana, kitu ambacho ni chukizo kwa Mungu.