WAAMINI KUWENI NA IMANI YA KWELI-ASKOFU MSONGANZILA


Waamini wa Jimbo Katoliki la Musoma wamekumbushwa kuacha kuchanganya imani mbili kwa wakati mmoja ,hali inayowapelekea kuamini masuala ya kishirikina na kuacha kumtegemea Mungu wanapokumbana na changamoto katika maisha yao ya kila siku.

Askofu wa Kimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila ameyasema hayo wakati wa kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa waamini zaidi ya 290 katika Parokia ya Mtakatifu Veronica Buhare Jimboni humo mei 07,2023 ,ambapo amesema ukomavu wa imani ndio silaha ya mambo yote hata unapopitia changamoto fulani.

“Wananngu kuweni na imani ya kweli hata kama ni ndogo kama mbegu ya haradali lakini hakikisheni mnasimama imara ndani ya imani mliyoikiri wakati wa ubatizo na Kipaimara, kwani Matukio ya kishirikina yamekuwa mengi sana ndani ya jamii zetu na haya ni matokeo ya dhambi,hebu acheni hizo imani potofu mrudieni Mungu na msimame imara katika Kristo na yote hayo mtayashinda ”amesema Askofu Msonganzila.

Askofu Msonganzila amesisitiza pia suala la kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu hasa kwa kushiriki semina mbalimbali ambazo zinawaimarisha kiroho kupitia wataalamu mbalimbali ikiwemo kufanya Hija binasfi na hata kikundi katika Kituo cha Kitaifa cha Huruma ya Mungu Kiabakari pamoja na Kituo cha Hija cha Nyakatende ambao ndiko Uinjilishaji ndani ya Jimbo letu ulikoanzia na kisha kusambaa ndani ya Jimbo zima.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Veronica Buhare Padri Novatus Shayo amemshukuru Mhashamu Askofu Michael Msonganzila kwa kukubali wito wake wa kufika Parokiani hapo na kuwaimarisha waamini wa Parokia hiyo kiimani kwa kuwapatia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa waamini zaidi ya 290.

Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Veronica Buhare George Mshomi amemshukuru Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila kwa kufika Parokiani hapo baada ya kukaa muda mrefu zaidi ya miaka 5 bila waamini kupata Kipaimara,na sasa waamini wameendela kukua kiimani hasa kwa kuendelea kupokea sakramenti mbalimbali za Ubatizo,Komunyo,kipaimara na hata ndoa.