MSAMAHA NI DAWA YA MAGONJWA-PADRI NKURUNZINZA


Wakristo nchini wametakiwa kuwa na moyo wa kusamehe ili kujiepusha na magonjwa yanayosababishwa na msongo wa mawazo kutokana na kupata majeraha ya moyo.

Hayo yamebainishwa na Wakili Paroko Padri Moses Nkurunzinza kwenye kongamano la Roho Mtakatifu linaloendelea katika Parokia ya Mtakatifu Veronica Buhare Jimbo Katoliki la Musoma,kuanzia Mei 19 hadi Mei 28 siku ya Pentekoste.

“Watu wengi sasa ni wagonjwa kutokana na majeraha ya moyo waliyonayo,mtu amejeruhiwa na ndugu yake,mme wake,baba yake na sasa kila anapokaa na kufikiria maumivu aliyoyapata kutokana na mtu fulani tayari anapata presha,miguu kuuma,madonda ya tumbo,kisukari na magonjwa mengine mengi,hivyo ili uwe salama lazima usamehe ” Amesema Padri Nkurunzinza.

Wakili Paroko amesema katika maisha ya mwanadamu kujaribiwa ni sehemu ya maisha na unapopata changamoto yoyote iliyosababishwa na mwanadamu usimuache Mungu,maana hata Yesu alijaribiwa, hivyo kinachotakiwa ni kufahamu namna ya kuuponya moyo wako na kumueleza Mwenyezi Mungu shida zote na kisha kusamehe,bila kusahau kujiweka karibu na Mungu ili uponye nafsi yako.

Amesema msamaha ni dawa ambayo imeponya magonjwa mengi bila hata kutumia wataalam wa sayansi hata unaposababishiwa majeraha na mtu wako wa karibu au uliyemuamini sana, kwa kuwa maamuzi ya kutoa msamaha yapo ndani ya mtu mwenyewe tofauti na kuanzia kutafuta vipimo vya kitabibu.

Akizungumzia kongamano hilo la Roho Mtakatifu Paroko wa Parokia hiyo padri Novatus Shayo amesema, lengo kubwa la kuandaa kongamano hilo lililoenda sambamba na novena ya Roho Mtakatifu ni kuwaandaa waamini wajiweke tayari kumpokea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste.