WAAMINI TUJITOE SADAKA KWA MAMBO YA MUNGU -PADRI CHEGERE


Waamini nchini wamekumbushwa kutumia nafasi walizonazo za ajira iwe serikalini au sekta binafsi kumtukuza Mungu kupitia matendo yao na kuacha Mungu awainue mwenyewe badala ya wao kujikweza.

Kauli hiyo imetolewa na Paroko wa Parokia ya Musoma Mjini Padri Medard Chegere wakati wa homilia ,ambapo amesema wakristo wanapaswa kuhakikisha nafasi walizopewa hata kama ni kubwa au ndogo hawaachi kufanya kazi ya Mungu.

“Tujifunze kupitia kwa wenzetu kuna watu wana nafasi Serikali na hata sehemu nyingine nzuri tu lakini wanajifanya wako bize(busy) hawataki kujisadaka, wanasahau kuwa nafasi waliyonayo wamepewa na Mungu,sisi wakristo tumtangaze Kristo kupitia matendo yetu,hata kama una cheo kikubwa usiache kufanya kazi ya Mungu maana ndiye anayekuwezesha na wala usijikweze acha Mungu akukweze mwenyewe ” amesema Padri Chegere.

Padri Chegere amesema ndani ya Jamii kuna mambo mengi ambayo waamini tunapaswa kuyatenda ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunawasaidia wahitaji ili Yesu anapopaa Mbinguni basi Roho Mtakatifu aliyetuahidi kutuachia, aweze kuendelea kutusaidia kututia moyo katika kuyatekeleza majukumu yetu.

Fazel Janja, muumini wa Kanisa kuu amesema kufanya kazi ya Mungu kunahitaji kutenga muda ili uweze kumtumikia na sio kuwa bize kama ambavyo mtu anatenga muda wake katika shughuli nyingine anazokuwa anazifanya katika sehemu yake ya kazi.

Mary Bhoke, amesema, sisi wakristo tuige mfano wa maisha ya Meja jenerali mstaafu Venance Mabeyo ambaye amekuwa mfano wa kuigwa na Waamini wengine, licha ya kuwa na nafasi kubwa Serikalini, alitenga muda wa kumtumikia Mungu na sasa tunashuhudia tunaona mpaka Baba Mtakatifu Francis ameona mchango wake katika Kanisa na kuamua kumpatia tuzo.