UPADRISHO NYAMONGO: Kazi ya padri si kuangamiza tu bali hata kupanda -Askofu Msonganzila


Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amesema, padri hapewi tu mamlaka ya kuharibu na kuangamiza chochote kinachopingana na Ufalme wa Mungu bali anapewa pia mamlaka ya kujenga na kupanda chochote kinachosimika Ufalme wa Mungu ili kukamilisha mpango wake.

Askofu Msonganzila ameyasema hayo wakati wa Misa Takatifu ya kutoa daraja takatifu ya Upadri kwa shemasi James Shelembi, iliyofanyika katika Parokia ya Mt. Rafael Malaika Mkuu Parokia ya Nyamongo Jimboni Musoma julai 20,2023, ambapo amemkumbusha Padri kufuata ushauri katika kufanya kazi ya Mungu huku akishirikisha moyo wake.

“ Mungu ana hati miliki juu yako kama alivyokuita na wewe ukaitika kuwa mhudumu wake,endelea kujiachilia mikononi mwake,mpe nafasi yeye aweze kukaa katika moyo wako ana akamilishe hitaji lako,na ukubali kuwa mhudumu wa kazi yake aliyokutuma ” amesema Askofu Msonganzila.

Akizungumza mara baada ya kupokea Sakramenti hiyo ya daraja Takatifu la Upadri, Padri James Shelembi amemshukuru Mungu kwa huruma yake amefanyika kuwa Padri, amemshukuru Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila kwa kukubali kumpatia sakramenti hiyo ya Upadri,na anawashukuru watu wote waliomuombea na kumuongoza mpaka kufikia siku hiyo aliyoitamani sana katika safari yake ya maisha mwenyezi Mungu awabariki sana.

Padri Shelembi amesema kazi yake ni kuwahudumia waamini kwa moyo wake wote na nguvu zake zote kulingana na mapenzi ya mwenyezi Mungu ya kuwa muhudumu ndani ya kanisa,na zaidi amewaomba waamini kuendelea kumuombea ili aweze kudumu katika hitaji lake la moyo.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo Nicodemus Kerayo amemshukuru Askofu Michael Msonganzila kwa kukubali kufika katika Parokia hiyo na kutoa daraja hiyo kwa Padri Shelembi kwani katika Parokia hiyo ni mara yao ya kwanza kutolewa kwa daraja hiyo.

Kerayo amewashukuru mapadri,masisita,waamini wote kutoka ndani na nje ya Parokia ya Nyamongo na Jimbo la Musoma kwa kufika na kushiriki pamoja katika adhimisho la Misa Takatifu ya Upadri katika Parokia hiyo,pamoja na majitoleo yao ya sala na fedha katika kufanikisha adhimisho hilo.