Wazazi Tuwalinde Watoto Wetu na Biashara Hii ya Binadamu-Ask. Msonganzila


Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuwajibika katika malezi ya watoto wao ili kuepuka kuwaingiza katika vitendo vya ya usafirishaji wa biashara haramu wa binadamu,pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo ni hatari kwa maisha yao.

Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila wakati wa kufungua semina ya siku moja iliyotolewa na shirika la Masista wa Mama Shauri jema Talithakum-TCAS ya namna ya kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu katika ukumbi wa shule ya msingi ya St. Michael iliyopo Parokia ya Sirari Jimbo Katoliki la Musoma mpakani mwa nchi jirani ya Kenya na Tanzania.

Katika semina hiyo ambayo imeshirikisha makundi ya watu mbalimbali katika jamii kama vile jeshi la polisi,uhamiaji,viongozi wa vijiji,viongozi wa kata,waratibu kata,Mapadri,masisita WAWATA, UWAKA, watoto na viongozi wa dini mbalimbali, Askofu Msonganzila amesema ,kuna kila sababu jamii kuiangalia biashara hii kwa jicho la kipekee sana kwa kuwa biashara hii ina madhara mengi sana kwa binadamu kama yalivyo madawa ya kulevya.

Tunashukuru shirika hili la Talithakum-TCAS linalosimamiwa na masista kwa kutuletea semina hii,ambayo inaendelea kutufungua zaidi hasa kwa wale tuliokuwa hatufahamu namna biashara hii inavyofanyika pamoja na madhara yake katika jamii,na sasa ni jukumu letu kama wana jamii kuhakikisha tunatoa taarifa za viashiria vyote vyauwepo wa biashara hii katika mazingira tunayoishi ili kukomesha kabisa biashara hii Amesema Askofu Msonganzila.

Sista Grace Mkosamali, Mratibu Msaidizi wa Talithakum-TCAS anasema lengo kubwa la kufika katika Parokia hiyo ambayo imepakana na nchi jirani ni kutaka kutoa elimu namna biashara hiyo inavyofanyika,pamoja na kuelezea sababu za biashara hii kuendelea kushamiri katika jamii zetu na madhara yake kwa wahanga,lakini pia namna ya kumsaidia mhanga.

Sista Mkosamali anatoa sababu za uwepo wa biashara hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa fursa za ajira,migogoro katika familia,migogoro ya kisiasa,umasikini,ukosefu wa fursa za kielimu,na ndoa za kushinikizwa na wazazi,ndugu na jamaa katika familia.

Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo Padri Respicius Kiiza amesema kazi ya kanisa ni kuendelea kukemea vitendo hivyo haramu ambavyo vinawakandamiza wanyonge wasioweza kujitetea ,kwani biashara hii ya ulanguaji wa binadamu haina faida mbele za Mungu.