Askofu Masondole: Acheni kukumbatia mila za kutakasa Wajane/ Wagane


Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda Simon Masondole amewataka wakristo nchini kuacha kukumbatia mila potofu zilizopitwa na wakati kwa kuwa mila hizo zinakwenda kinyume na mpango wa Mungu katika Kumuumba mwanadamu.

Askofu Masondole ameyasema hayo wakati wa Misa Takatifu ya harambee kwa ajili ya ujenzi wa kanisa katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji Nyamiongo, Jimbo katoliki la Musoma. Amesema kuwa ni aibu sana kuona wakristo wengi licha ya kubatizwa na kumkiri kristo, bado wamekumbatia mila hizo.

Ni tetemeko gani la kiimani ambalo linakupitia wewe Mkristo hadi unaamua kukumbatia mila hizo za nyumba ‘ntobhu’,za kuoa wake wengi na mwanamke kuoana na mwanamke mwenzako kwa ajili ya kupata watoto kwa njia isiyo harali? Au mtu amefiwa mke au mume harafu anatafutwa mtu wa kumtakasa, unajua aliyekufa alikuwa na maradhi gani,tokeni huko maana ya kubatizwa ni kuyaacha yote yasiyompendeza Mungu amesema Askofu Masondole.

Mkuu wa mkoa wa Mara ambaye amemuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Phillip Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo amesisitiza suala la wananchi kuchapa kazi kwa ajili ya kujiletea maendeleo ili kuepuka kujiingiza katika makundi mabaya na mila zilizopitwa na wakati,lakini pia kuacha tabia ya kukaa katika nyumba za ibada bila kufanya kazi.

Akitoa neno la shukrani Paroko wa Parokia hiyo Padri Chukwuemeka Anyanwu amewashukuru wageni wote waliofika kuwaunga mkono katika ujenzi wa Kanisa hilo pamoja na kukubali kupokea mwaliko wao wa kushiriki harambee hiyo.

Paroko huyo amemshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali wito na kutumia mwakilishi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Mohamed Said Mtanda kwani ameonyesha Upendo wa hali ya juu kwa waamini wa Parokia hiyo na wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ujumla.