Kiabakari: Askofu Msonganzila afungua jengo la kitega uchumi cha WAWATA, awaasa kushirikishana ujuzi


Flowers in Chania

Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wametakiwa kuwasaidia wanawake wengine katika kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuwasaidia kuinua kipato chao cha familia na taifa kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa jengo la kitega uchumi cha WAWATA JUBILEE COMPLEX katika Parokia ya Huruma ya Mungu Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma, Askofu wa Jimbo hilo Michael Msonganzila amesema wanawake wanapaswa kufundishana mbinu mbalimbali za kujiingizia kipato, ili kuondokana na utegemezi ndani ya familia na hata ndani ya kanisa.

Mama zangu washirikisheni wanawake wengine katika Parokia nyingine mbinu mlizotumia kupata wafadhili hadi mmefikia hatua hii kubwa ya maendeleo ya kupata kitega uchumi kikubwa na cha kisasa kwa ajili ya Parokia zenu na familia zenu lakini,kutengeneza ajira kwa jamii inayowazunguka,huu ni ubunifu mkubwa sana hongereni Amesema Askofu Msonganzila.

Askofu Msonganzila amewataka akina mama ambao katika Parokia zao hawajaweza kupata kitega uchumi cha kuwasaidia katika kuinua kipato chao basi wafike katika Parokia ya Huruma ya Mungu Kiabakari wajifunze hata kama hawataweza kuwa na mradi mkubwa kama wa kiabakari basi wanaweza kuanza na kidogo wanachoweza kusimamia kulingana na mazingira yao.

Paroko wa Parokia hiyo Padri Adam Wojciech amewashukuru akinamama wanne waliojitoa kwa ajili ya wanawake wengine hadi kufanikisha kupatikana kwa mradi huu mkubwa ambao utasaidia kuinua kipato cha akinamama wengine,na kuongeza ajira.

Akisoma taarifa ya mradi huo katibu Msaidizi wa WAWATA Parokia ya Kiabakari Flora Jacob amesema wazo la kuanzishwa kwa mradi huo ni baada ya kuona hali ya kipato cha akina mama iko chini kulingana na mazingira yao, ndipo walipoamua kumshirikisha baba paroko ili awasaidie kupata wafadhili ambao wataweza kuwajengea kitega uchumi cha kudumu kitakachopunguza hali ya umasikini katika familia zao na kuondokana na utegemezi kwa Kanisa, na Paroko aliamua kuwatafutia wafadhili kutoka nchini kwao Poland na kufanikisha kupatikana kwa mradi huo mkubwa na wa kisasa.

Wanawake hao wamemshukuru na wanamuombea maisha marefu na Utume mwema baba Paroko Wojciech kwa kuwasaidia kupata kitega uchumi hicho ambacho kitawasaidia mahujaji wanaofika katika Parokia hiyo kwa ajili ya Hija kila mara kupata huduma mbalimbali kama vile chakula,malazi,vinywaji,salon na huduma za kifedha ambazo zitakuwa zinapatikana katika kitega uchumi hicho.