Padri Luzangi alaani mauaji ya Angelo Malima

12/september/2023

Padri Benedicto Mukama Luzangi amelaani vikali mauaji ya kikatili yanayoendelea nchini kwa vijana wasio na hatia,ambayo yanasababishwa na marehemu hao kudai haki zao,na kisha kutendewa ukatili ambao unasababisha wao kupoteza maisha.

Padri Luzangi amelaani kitendo hicho wakati wa Homilia ya Misa ya Marehemu Angelo Malima kijana Mkatoliki (Kiwawa)kutoka Parokia ya Kristo Mfalme Rwamlimi Jimbo Katoliki la Musoma ambaye alifariki dunia baada ya kuchomwa na kisu sehemu ya moyo wakati akidai haki yake,kutokana na kuibiwa mara kwa mara.

hapana hapana tunahitaji wakati fulani kuwa na moyo wa subira,hatupasiwi kufumbia macho mauaji haya na wala hatuungi mkono kabisa tunalaani vikali ,hata kama mtu mtatofautiana katika majibizano ,msijichukulie sheria mkononi ,lazima tuwe na mazungumzano yanayoleta amani,hata kama tutatofautiana katika fikra zetu na sio kuleta madhara ya kupoteza uhai wa mtu amelaani vikali Padri Luzangi.

Padri Luzangi amewaomba wanajumuiya na waamini wote kuwa na mahusiano mazuri baina yao ,na kuacha tabia ya kulipiza kisasi au kujengeana chuki jambo ambalo sio zuri, bali wanapaswa kuwa na mazungumzo ya kirafiki hata kama unataka kuminya haki ya mtu basi jitahidini sana msilete madhara ya mauaji ,tumuombe Mungu atuepushe na moyo wa namna hiyo.

Akisoma wasifu wa marehemu Angelo George Malima kaka wa marehemu Josephati Malima amesema marehemu Angelo mnamo Septemba 8,2023 majira ya saa mbili usiku mita 20 kutoka nyumbani kwao alichomwa na kisu sehemu ya moyo na vijana waliosadikika kumuibia nyavu zake ziwani,na katika majibizano yao ndipo mmoja alifanya unyama huo na kupelekea kuvuja damu nyingi.

Amesema walimkimbiza katika Hospitali ya Mkoa wa Mara ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Kwangwa wakati wanaendelea na jitihada za kutaka kuokoa maisha yake Angelo Malima alifariki dunia.

Akizungumza kwa niaba ya familia Padri Peter Malima amewaomba waamini kuendelea kumuombea ndugu yao marehemu ili apate pumziko la Milele mbinguni lakini kuwaombea wao waliobaki kwani ni kipindi kigumu sana walichonacho na bila neema ya Mungu peke yao hawawezi kitu.

Angelo George Malima ndiye kijana wa kwanza aliyehamasisha michezo kwa viwawa katika Parokia ya Rwamlimi na alikuwa ni mchezaji wa mpira katika Timu ya Baruti FC,Biashara United ya Mkoa wa Mara na Tunduru Masasi Kusini,ambapo alifanikiwa kuleta vikombe vingi vya ushindi katika timu hizo

.

BWANA AMETOA NA BWANA AMETWA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE AMINA.