Askofu Sangu awasihi wanawake kuacha ukatili kwa Watoto

20 September, 2023

Flowers in Chania

Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga Liberatus Sangu amelaani vikali vitendo vya ukatili kwa watoto vinavyoendelea kwa akina mama hasa kwa kujifungua watoto na kuwatupa, kitendo ambacho ni cha kinyama na hakifai mbele za Mungu.

Askofu Sangu ameyasema hayo wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya uzinduzi wa Gorotho la Yesu wa Ekaristi katika kituo cha kulelea watoto cha Bikira Maria Mama wa Mungu Msaada Daima Lamadi Busega ,ambapo amesema kujifungua na kutupa mtoto huo ni zaidi ya ukatili walio nao wanyama kwa kuwa sasa hivi binadamu hathamini kabisa suala la Uumbaji.

Inasikitisha sana kuona watoto wanakuwa chukizo na sio Baraka tena na nyakati hizi mambo yamekuwa mengi sana ukatili dhidi ya watoto ni mkubwa sana ,watu wanahangaika kwa waganga kutafuta watoto ila sisi tunawakatili na kuwatupa, hapana tusifanye hivyo, watoto wanaokotwa tayari wakiwa wameshaanza kushambuliwa na wadudu (sisimizi) na wengine wanathubutu kutupa watoto wakiwa bado hawajafikia umri wa kuzaliwa. Wanatoa mimba wanatupa chooni,nawaomba tuwe watetezi wa uhai wa binadamu Amesema Askofu Sangu.

Amesema haijalishi mtoto huyo kapatikana kwa njia gani na kama Mama Bikira Maria angemtupa Yesu sijui ni nani angetukomboa tena kwa kutoa uhai wake,tunapaswa kujifunza kutoka kwake kwani mtoto ni Baraka na sio laana tuwapokee na tuwalee kulingana na mafundisho ya Yesu,na huo ndio wajibu wetu kama wakristo ambao kila mara tunasisitiza kutunza na kulinda uhai.

Mkurugenzi wa Kituo hicho Sista Helena amesema kuwa wanao watoto wengi kutoka Pugu,Mwanza,Lamadi na Musoma ambao kituo hicho kinawapokea na kuwasaidia kulingana na changamoto mbalimbali wanazokuwa nazo,na wengine wamekuwa wakiwapokea wakiwa na hali mbaya na wengine wanakufa kutokana na kuchelewa kupelekwa kituoni hapo baada ya kutupwa au kutelekezwa na wazazi wao.

Sista Helena amesema kanisa katoliki ni kanisa linalotetea uhai wa mwanadamu na hata anayetupwa au kutelekezwa na wazazi au familia ana chumba pale,kwani Yesu anasema wote wenye kuelemewa na mizingo wamfuate yeye,na yeye kwa kushirikiana na akina mama wanao msaidia kulea watoto hao wako tayari kuwasaidia watoto wanaoteseka kuliko kufanyiwa ukatili na hata kupoteza uhai wao.