Katibu Elimu Jimbo la Musoma,Pd. Julius Magere, awaasa Wanafunzi kuzingatia maadili wanayofundishwa shuleni

26/september/2023

Wanafunzi wanaohitimu darasa la saba na kidato cha nne, wamekumbushwa kuhakikisha wanazingatia malezi na maadili mema waliyofundishwa walipokuwa shuleni wanayaendeleza ili kuwa mfano bora kwa jamii, lakini pia kuwa kioo katika kutangaza taasisi walizosomea.

Hayo yamesemwa na Padri Julius Magere Paroko wa Parokia ya Serengeti Jimbo Katoliki la Musoma, na Katibu wa Elimu Jimbo,wakati wa mahafali ya 18 ya wanafunzi wa awali na darasa la saba wa shule ya Milenia ya tatu Masonga Jimboni humo,kuwafikisha siku hiyo baada ya kukaa shuleni kwa miaka zaidi ya 7 kuanzia elimu ya awali hadi ya darasa la saba.

Padri Magere amesema kwa muda wa miaka waliyokuwa shuleni wamekuwa na nidhamu na maadili mema ambayo yamekuwa kivutio kwa wengine,na taasisi za kanisa zimekuwa mfano wa kuigwa kwa malezi hivyo ni bora wakayaendeleze ili kumtangaza Kristo katika matendo.

Tunawashukuru wote kwa muda ambao tumekuwa wote na sasa mnaondoka katika taasisi zetu,haitapendeza tukisikia kuwa mtoto fulani aliyesoma katika shule fulani inayosimaiwa na kanisa anahusishwa na mambo maovu maovu huko mtaani kama ya kulewa kupindukia,wizi,uvutaji wa bangi na madawa ya kulevya hapana hatutaki kusikia hivyo kuweni mfano bora kwenu wenyewe na kwa taasisi zilizowapika hadi mkaiva kimaadili na kiroho,amesema Padri Magere.

Padri huyo amewakumbusha wazazi pia kuwajibika kwa watoto ipaswavyo katika kipindi hiki ambacho sasa wanakwenda kukaa nao kwa muda wakisubiri matokeo yao ya mtihani ambayo wanaamini kuwa wote watafaulu kulingana na namna walivyofundishwa na kufanya mazoezi mengi,kuhakikisha wanatenga muda wa kutosha wa kukaa nao ili kuwafahamu watoto wao vizuri kitabia na kimwenendo na sio kuwaachia wenyewe wajilee bila kudhibitiwa.

Msimamizi wa shule hiyo, Sista Irene Loina Kaibunga wa shirika la Incarnate Word sisters ambao ndio wasimamizi wa shule hiyo amewashukuru wanafunzi na wazazi kwa kuwaamini na kuwaleta watoto wao katika Shule ya Milenia ya tatu Masonga kwani watoto wao wanapata elimu bora ya kiroho na kimwili,lakini wanazingatia maadili na tamaduni za kitanzania.

Kaimu Afisa elimu awali na msingi Wilaya ya Rorya Paulin chacha ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kuwa ni moja ya shule ndani ya Wilaya hiyo inayofundisha vizuri maadili kwa kuzingatia mwongozo wa Serikali na ya Kanisa.