Tumieni muda wa kutosha kuchungunzana na mwenzi wako kabla ya kufunga ndoa- Pd. Chacha

27/september/2023

Wanaotarajia kufunga ndoa (wachumba) nchini wamekumbushwa kuchunguzana kwa kina na kwa muda mrefu kabla ya kufanya maamuzi ya kufunga ndoa ili kuwasaidia kuishi agano la Mungu kwa kuzigatia mwongozo wa kanisa wa kutenganishwa na kifo.

Ndoa nyingi kwa sasa zimekuwa ni ndoano kulingana na wanandoa wengi kukutana ndani ya wiki moja na kufanya uchumba wa miezi michache na kisha kufunga ndoa hali inayosababisha ndoa nyingi kuvunjika mara baada ya kila mmoja kumfahamu vizuri mwenzake.

Hayo yamebainishwa na Paroko wa Parokia ya Tarime Jimbo Katoliki la Musoma Padri Lucas Chacha wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu kwa kuwafikisha siku hiyo ya kutimiza miaka 50 ya ndoa ya Mzee Stanslaus Sabure na Maria Nyarugendo, Misa imefanyika nyumbani kwao katika Parokia Teule ya Kiongera na kuongozwa na Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila.

Padri Chacha amesema kumekuwepo na changamoto kubwa sana ya kuomba kutengana mara baada ya kufunga ndoa takatifu hali inayoashiria maandalizi mabovu ya kipindi cha uchumba kabla ya kufanya maamuzi ya kuishi pamoja.

Nataka niseme ukweli katika migogoro mingi inayotuhangaisha maofisini kwa sasa ni migogoro ya wanandoa wakiomba kuachana,sasa unajiuliza hawa wana muda mfupi ndani ya maisha ya ndoa lakini kwa nini wanaomba kuachana, majibu unakuta kwamba uchumba wao waliufanya aidha kwa njia ya mtandao au walikutana ndani ya miezi michache tu na kufanya maamuzi ya kuoana na haya ndio matokeo yake Amesema Padri Chacha

Akizungumzia siri ya kufikisha miaka hiyo ya ndoa mzee Stanslaus Sabure ambaye ni baba wa Padri Cleophas Sabure wa Jimbo la Musoma amesema, sio kwamba hakuna changamoto walizokutana nazo hadi kufikia siku hiyo, lakini moja ya siri kubwa ni kuvumiliana katika taabu na raha, lakini pia upendo wa dhati .

Mzee Stanslaus Sabure amewashukuru wote waliofika katika kusherehekea jubilei yao ya miaka 50 ya ndoa ,ambapo kwa miaka ya sasa ni ngumu sana vijana wengi kufikisha miaka hiyo.

Amewaasa vijana wa sasa kuacha kuingia katika ndoa kwa sababu ya shinikizo la wazazi,ndugu na jamaa bali waingie baada ha kuchunguzana kwa muda na kuwashirikisha wazazi ili kuwasaidia kufatilia mienendo ya maadili katika familia husika.