Hongereni kwa mshikamano mlio nao wana kiongera- Askofu Msonganzila

28/september/2023

Flowers in Chania

Waamini wa Parokia Teule ya Kiongera Jimbo Katoliki la Musoma wamepongezwa kwa kuendelea kuwa na umoja,upendo na mshikamano katika kujiletea maendeleo katika Parokia yao,kutokana na kufanya mambo makubwa ya maendeleo ndani ya muda mfupi, baada ya kutangazwa kuwa Parokia Teule.

Pongenzi hizo zimetolewa wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini zaidi ya 370 wa Parokia hiyo na Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila wakati wa ziara yake ya kichungaji katika Parokia hiyo hivi karibuni.

Askofu Msonganzila amesema kwa muda mfupi sana waamini wameweza kufanya mabadiliko makubwa ya kimaendeleo,hali inayoonesha ukomavu wa kiimani kwa waamini,lakini pia uaminifu katika kusimamia kile kinachopatikana kutokana na majitoleo yao.

Naomba niwapongeze kwa moyo wa dhati kabisa,mabadiliko ni makubwa sana na haya yote yanatokana na mshikamano mlionao, bila umoja na mshikamano hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana,endeleeni na umoja huo na Mwenyezi Mungu abariki kazi za mikono yenuamesema Askofu Msonganzila.

Paroko wa Parokia hiyo Padri Athanas Zengo OSA amemshukuru baba Askofu kwa kukubali kufika katika Parokia hiyo na kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa waamini hao na kuwatia moyo katika Utume,kwa kufika kwake kunaongeza zaidi mwamko katika imani.

Padri Zengo amewashukuru pia waamini wote wa Parokia Teule ya Kiongera kwa mshikamano walionao katika kujitoa sadaka kwa kazi ya Mungu na kuwaomba kamwe wasirudi nyuma katika kumtolea Mungu sadaka, kwani majitoleo hayo ni hazina mbinguni.