Askofu Msonganzila: Usiwe Kikwazo Kwa Wengine Kama Unataka Kufanikiwa

06/11/2023

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila amewakumbusha waamini nchini kuacha tabia ya kuzuia mafanikio ya watu wengine, hasa pale wanapotakiwa kusaidia wahitaji au kutoa msaada wa jambo fulani kwa watu wengine.

Askofu Msonganzila ameyasema hayo Novemba 5, 2023 wakati wa homilia katika Parokia ya Mt. Fransisko wa Asizi- Mugumu ambapo amesema, Kama unataka kuwa na mafanikio tembea na watu,huwezi kufanikiwa ukiwa sehemu ya kutengeneza vikwazo kwa watu wengine, watu wanapohitaji msaada wako wasaidie kadri uwezavyo na wasiishie kusikitika tu na kuwa na manug'uniko mioyoni mwao.

Amesisitiza kuwa maisha yetu kila siku ni elimu huwezi kufanikiwa kama unanungunikiwa na watu,tunafundishwa kupendana, kuheshimiana,kusaidiana katika hali zote,mwenye nacho na asiyekuwanacho kwa kuwa mafanikio ya mtu yeyote yanahitaji ushirikiano na watu mbalimbali, hivyo pale unapoombwa msaada na unauwezo wa kusaidia ni jambo nzuri kuwa tayari kutoa.

Askofu Msonganzila amewapongeza waamini wa Parokia hiyo kwa ushirikiano walionao hasa katika kujiletea Maendeleo na amewasihi waendelee kudumisha mshikamano huo na kamwe wasiwe sehemu ya vikwazo kwa wengine. Aidha,Paroko wa Parokia hiyo Padri Joel Marwa amemshukuru Baba Askofu kwa kufika katika Parokia hiyo na kuwapa ujumbe ambao unazidi kuwaimarisha zaidi kiimani.