Tukosoane kwa Haki na Upole na sio kwa Kufokeana - Pd. Luvakubandi

21/11/2023

Wakristo wanatakiwa kuwakosoa watu wanaowaona wamekosea iwe kwa kujua au kutokujua, kwa kutumia hekima na busara pasipo kuharibu au kumchafua mtu.

Akizungumza wakati wa misa kwa wafanyakazi wa makao makuu ya Jimbo, Padri Robert Luvakubandi amesema kuwa hakuna binadamu aliyekamilika bali kila mtu ana mapungufu yake hivyo mtu anapokosea katika jambo fulani basi hakuna budi kumkosoa kwa hekima ili kuendelea kulinda heshima na utu wake.

Tunaishi katika jumuiya yenye changamoto za kila aina, hakuna aliyekamilika, kinachotakiwa kwa mwenzako ni kumkosoa kwa kulinda haiba yake kwani wengine wanapomuona mtu kakosea huenda na kumkosoa kwa kumtukana bila hata kujua ana hali gani kwa wakati huo, huenda kavurugwa au kapatwa na jambo ambalo hata yeye hawezi kukumbuka kwa wakati huoamesema Padri Luvakubandi.

Amewataka waamini na jamii kwa ujumla kuishi maisha ya msamaha na unyenyekevu ili kujenga jumuiya yenye furaha,amani na upendo kwa kuwa wote hapa duniani tu wasafiri hakuna aliye na maisha ya kudumu,hivyo ni vema kukosoana kwa hekima na upendo.

Padri Luvakubandi amesema ili ukomae katika jambo fulani ni lazima ufanye makosa ili kuwa imara zaidi,chakujifunza ni kwamba unapogundua umekosea basi ni vema ukaomba msamahaha ili kuwa mnyenyekevu na mwenye hekima kama ya mzee Suleimani.

Amewaomba watumishi wote walio na nafasi mbalimbali katika taasisi kuhakikisha wanatenda jambo kwa upendo na ukarimu kwa watu wanaowahudumia ili kumtangaza Kristo.


    Latest News