Nawashukuru Waamini wa Jimbo La Musoma Kwa Majitoleo Katika Uinjilishaji -Askofu Msonganzila

28/11/2023

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewapongeza waamini wa Jimbo hilo kwa majitoleo yao ya hali na mali katika kuendeleza shughuli za uinjilishaji na maendeleo ya ustawi wa jamii ndani ya Jimbo.

Askofu Msonganzila ameyasema hayo wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya kufunga mwaka wa kanisa na siku ya Missio -Musoma Novemba 26,mwaka huu,katika Kanisa kuu la Maria Mama wa Mungu Musoma mjini,ambapo amesema majitoleo yao yameendelea kusaidia katika kutangaza neno la Mungu.

Niwashukuru walei wote kwa namna mnavyoshikamana katika kazi ya uinjilishaji,kwa mwaka jana tulipata zaidi ya millioni 40 siku ya Missio -Musoma na imesaidia sana katika kujenga vigango vilivyokuwa vimekaa muda mrefu bila kukamilika na waamini walikuwa wanatembea umbali mrefu katika kufata huduma ya kiroho,tumesomesha masista na mafrateli pamoja na kuwasaidia kununua usafiri kwa ajili ya Padri ambao hawakuwa na usafiri ili waweze kufanya Utume wao vizuri,hilo sio jambo dogo nawashukuru sanaamesema Askofu Msonganzila.

Askofu huyo amesema katika kujenga hekalu la Mungu lazima kila mmoja ajitolee, maana hakuna mtu asiye na kitu cha kutoa na unapojitoa kwa moyo wote kwa ajili ya kazi ya Mungu,mwenyezi Mungu huwa anakurudishia mara dufu hivyo tusijione wanyonge tunapoambiwa kusaidia shughuli za uinjilishaji.

Paroko wa Parokia hiyo Padri Medard Chegere amemshukuru Mhashamu Baba Askofu kwa kukubali kuadhimisha Misa Takatifu ya siku ya kufunga mwaka wa kanisa na Missio -Musoma katika Parokia hiyo pamoja na kuwapatia waamini neno la kuwatia moyo na hamasa juu ya majitoleo katika kazi ya uinjilishaji.


    Latest News