Walimu msikaririshe wanafunzi-Askofu Msonganzila


Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewataka waalimu wa shule za msingi na sekondari kuacha tabia ya kuwakaririsha wanafunzi kwani kufanya hivyo ni kuwafanya wasiwe na uwezo wa kujiamini wao wenyewe huku wakiwa na matokeo mazuri lakini uwezo wa kujieleza wakiwa hawana.

Akizungumza wakati wa Misa Takatifu ya uzinduzi ,kubariki wanafunzi na majengo ya shule ya sekondari ya Little Flower ambayo imeanza mwaka wa kwanza mwaka huu ikiwa na wanafunzi 111 Askofu Msonganzila amesema kuwa kitendo hicho ni kumfanya mwanafunzi asiwe na uwezo wa kujieleza mwenyewe wakati matokeo yao ni mazuri, .


kukaririsha wanafunzi hapana ,kama mtoto hana uwezo mnaouhitaji basi anzisheni twisheni ili kumsaidia na nsio kukaririsha,lakini niwapongeze wana Mugumu hii ni hatua nzuri kuanzisha shule ya awali,msingi hadi sekondari ,Majitoleo yenu yanayotia moyo sana, kuna shule ndani ya Jimbo hili tangu wanaanza ni shule ya awali na msingi tu mpaka kesho hawajawahi kufikilia kuwa na shule ya sekondari wala chuo ,mimi nawapongeza sana kwa majitoleo haya Amesema Askofu Msonganzila.

Paroko wa Parokia ya Mugumu Padri Joel Marwa amesema kuwa mpaka kukalika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa,vyoo ,maabara ,mabweni ya wasichana na wavulana , miundombinu ya maji na umeme zaidi ya shilingi milioni 319 zimetumika ikiwa ni michango iliyotokana na shule ya msingi ya Little flower pamoja na mchango wa milioni 32 kutoka Ofisi ya baba Askofu wa Jimbo hilo.

Padri Joel amesema mchakato wa ujenzi ulianza Mei 2019 na ujenzi rasmi ulianza julai 2019 na hadi kufikia Januari 2020 miundombinu yote ilikuwa imekamilika ikiwemo vyumba 8 vya madarasa,ofisi mbili ,jengo la utawala,maabara vyumba 3,matundu 16 ya vyoo,mabweni 2,makitaba 1,kuweka umeme katika eneo la shule,kuchimba visima 2 virefu na jiko moja.

Mkuu wa Udekano wa Serengeti Padri Medard Chegere amesema wamefurahi sana kupata shule hiyo kutokana na ushirikiano uliopo baina ya wananchi wa eneo hilo,waamini na Serikali kwani nguvu ya pamoja ndio ilifanikisha suala hilo hadi kukamilika kwa ujenzi na miundombinu yote ya shule hilo na hivyo kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu amelishukuru Kanisa Katoliki kwa kuwa mstari wa mbele katika suala la elimu hasa katika kupambana na adui ujinga na maradhi kwani shule hiyo imefikisha idadi ya shule za sekodari katika wilaya hiyo 41 na ni shule ambayo itasaidia watoto wengi kupata elimu bora karibu kuliko walivyokuwa wakisafiri umbali mrefu.

Babu ameliomba Kanisa kufikiria kujenga Chuo kikuu katika Wilaya hiyo,huku ameahidi kushughulikia suala la ulinzi na usalama wa wanafunzi na miundombinu ya barabara inayoenda katika shule hiyo kutoka mjini hadi shuleni hapo ,kwani Kanisa limekuwa likishirikiana bega kwa bega na serikali hata katika masuala ya ukatili wa kijinsia limekuwa mstari wa mbele katika kukemea na hivyo baadhi ya matukio ya uharifu yamepungua japo madogomadogo bado yapo.

Kwa upande wao wananchi wa Wilaya hiyo wamelishukuru Kanisa kwa kujenga shule hiyo kwa awali wazazi walikuwa wanasafirisha wanafunzi umbali mrefu na hata wakati mwingine changamoto ya mahitaji ya wanafunzi kutokana na umbali ,lakini kwa sasa watoto wao watasoma karibu na nyumbani.