Wanawake Wanaohudumia Familia Zao Wenyewe ni sawa na Wajane-Padri Chegere

01/02/2024

Imeelezwa kuwa mwanamke anayesimamia majukumu yote katika familia huku akiwa na mwanaume ambaye hawajibiki katika kusimamia majukumu yake kama baba ndani ya familia ni sawa na kuitwa mjane,kwa kuwa anayepaswa kubeba majukumu ya familia yupo na hawajibiki na wala hana msaada wowote.

Hayo yamesemwa na Paroko wa Parokia ya Maria Mama wa Mungu Kanisa kuu Musoma Mjini Padri Medard Chegere Januari 28,2024 ambapo amesema wanaume wengi wamesahau majukumu yao na wamewaachia wake zao kusimamia majukumu ya familia hali ambayo haina utofauti na mwanamke aliyefiwa na mume.

Wanawake mnaohudumia familia zenu peke yenu bila kusaidiwa na waume zenu wanapoita wajane muwe wa kwanza kwenda mbele maana hamna tofauti na wajane,tofauti yenu na wajane halisi ni kwamba wao waume zao walishatangulia mbele za haki ila ninyi waume zenu wapo na hawawasaidii chochote katika majukumu ya familia amesema Padri Chegere.

Padri Chegere amesema hali inazidi kuwa mbaya kutokana na ukweli kuwa wanaume wengi wameacha kuwajibika na hivyo mzigo mkubwa wa malezi unawaangukia akina mama ambao muda mwingi ndio wanaokuwa karibu na watoto na hivyo watoto wanakuwa na malezi ya upande mmoja tu.

Ni ngumu sana mama kumuangalia mwanae analia kwa sababu ya kukosa chakula huku akimsubirilia baba ambaye ameaga toka asubuhi hadi jioni hajaonekana ili alete chakula watoto wale,hii ndio inayowafanya wajishughulishe zaidi huku na kule ili watoto wapate chakula kwa wakatiamesema Padri Chegere.

Amewakumbusha wanaume kuhakikisha wanashirikiana na wake zao ili kurahisisha mambo mbalimbali ya kimaendeleo katika familia na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri hata katika jamii inayowazunguka na zaidi kuwa na familia iliyobora,kuanzia katika malezi ya watoto wao.