Tuwaruhusu Watoto wetu Wajiunge na Utawa - Askofu Msongazila

08/02/2024

Wazazi/walezi wametakiwa kuacha tabia ya kuwakatisha tamaa watoto wanaotamani kuingia katika wito wa Utawa na Upadri kwa kuwaambia maneno makali na yasiyompendeza Mwenyezi Mungu na hivyo wanashindwa kufikia ndoto yao ya kumtumikia Mungu katika miito hiyo.

Flowers in Chania

Kauli hiyo imetolewa na Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila wakati wa Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu kwa jubilee ya miaka 50 ya utawa kwa Sista Rozalia Mgaho wa Shirika la Kazi za Roho Mtakatifu katika Parokia ya Iramba.

Baba zangu na mama zangu tuwaache watoto wetu wanaotamani wito huu waingie ili wamtumikie Mwenyezi Mungu,kwani mnafikiri wanaokuwa mapadri na masista hawana vipawa vingine? Wanavyo, isipokuwa kila mtu na kipendacho roho, waacheni msiwakatishe tamaa kwa kuwaambia maneno ambayo hayampendezi Munguamesema Askofu Msonganzila.

Aidha, Askofu Msonganzila amewaomba vijana wa kiume na kike kujiunga na miito ili kuongeza idadi ya wahudumu kwa ajili ya kuwahudumia kondoo wa Mungu kwani zizi lisilokuwa na ndama linaisha haraka, hivyo amewaasa wazazi waendelee kuwahamasisha watoto wao kujiunga na miito ya upadri na utawa ili tuweze kuwa na wahudumu wengi.

Paroko wa Parokia ya Iramba Padri Samson Awach amemshukuru Mhashamu baba Askofu kwa kukubali kufika katika Parokia hiyo na kuongoza Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa miaka 50 ya utawa wa sista Rozalia,ambaye amelitumikia Kanisa kwa miaka hiyo,bila kukata tamaa.

Akitoa neno la shukrani Sista Rozalia amesema kufikisha miaka 50 ya utawa haikuwa kazi rahisi isipokuwa kwa mapenzi ya Mungu, kwani wengi aliyoanza nao safari ya wito huo, hawakufika wote, hivyo anamshukuru Mungu kwa kuendelea kumpatia afya njema ya roho na mwili ili aendelee kumtumikia kadri apendavyo yeye.

Amemshukuru Mhashamu Baba Askofu kwa kukubali kufika na kusali pamoja na waamini wa Parokia ya Iramba ambao wamekuwa naye bega kwa bega katika kumtia moyo wakati wote wa Utume wake bila kuchoka,huku akiwaomba waamini wote kuendelea kumuombea ili atimize kazi ya Mungu hadi mwisho wa safari yake ya hapa duniani.