Waamini Endeleeni Kutuombea-Askofu Msonganzila

26/03/2024

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewaomba waamini kuendelea kuwaombea mapadri ili waendelee kuwa faraja kiimani na wala wasiwe kikwanzo,majeraha au chanzo cha kutawanya waamini bali wawe chanzo cha kuwaunganisha waamini.

Hayo ameyasema wakati wa homilia ya kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya kubariki mafuta ambayo imefanyika Kanisa kuu la Maria Mtakatifu Mama wa Mungu Parokia ya Musoma mjini machi 26,2024 na kwamba ni vema kuzingatia dhamana waliyopewa na Mwenyezi Mungu ya kuwa walinzi wa hazina ya Kanisa.

Askofu amesema siku ya kubariki mafuta ni siku maalum kwa Mapadri kukumbuka siku ya daraja Takatifu la upadri na ndio maana kila wanapobariki mafuta ya Krisma Takatifu ni lazima warudie ahadi zao kwa lengo la kujiingiza katika kazi ya kujitakatifuza na kujiimarisha zaidi kiimani.

Flowers in Chania

hii siku ni yetu kwa mpango wa kanisa na Mungu, tumepewa dhamana ya kuchunga makundi mbalimbali hivyo ni vema tukatambua nafasi yetu kuwa kazi hizi tatu tunazifanya kwa niaba ya Yesu Kristo mwenyewe ambaye ndiye aliyeanzisha kazi hii,tusiwe kikwazo katika kuadhimisha mafumbo haya"amesema Askofu Msonganzila.

Askofu Msonganzila amewakumbusha Mapadri kujinyenyekesha wakati wa kufundisha kwa kuwa kazi kubwa waliyopewa na Mungu ni kufundisha,kutakatifuza na kuchunga kondoo waliokabidhiwa bila kusahau kuwa sehemu ya furaha katika jumuiya, Parokia na taasisi zote kwani wamepakwa mafuta ambayo ndio kielelezo chao.

Amewashukuru waamini wa jimbo hilo kwa kuendelea kuwa kitu kimoja katika kulitangaza neno la Mungu na hasa katika majitoleo yao ambayo ndiyo yanayoiwezesha kazi ya Mungu kusonga mbele na kuwaomba waendelee kushikamana katika kulitangaza neno la Mungu na kuwatia moyo.

Josia kigaza Muumini wa Parokia hiyo amemshukuru Mhashamu Baba Askofu kwa kuadhimisha Misa Takatifu ya kubariki mafuta ya Krisma ambapo amesema daima wataendelea kushikamana ili kusukuma gurudumu la uinjilishaji ndani ya Kanisa Katoliki.