Askofu Msonganzila atoa tahadhari ya Corona

16/03/2020

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewataka waamini na wananchi wa Jimbo hilo, kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Corona kwa kuhakikisha wanafuata kanuni za afya zinazotolewa na Wizara husika.
Akizungumza Ofisini kwake Machi 16 mwaka huu,Askofu huyo amesema kutokana na taarifa mbalimbali kutoka kwenye vyombo vya habari ,huku ugonjwa huo ukiwa umeshafika nchi jirani ya Kenya ,kuna haja ya kila mtu kuchukua tahadhali kulingana na mwingiliano wa watu. .

Nashauri Parokia zote na Jumuiya mbalimbali za Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, kuchukua baadhi ya hatua za Tahadhari kama vile mpangilio wa watu kukaa Kanisani ,uwe mzuri kwa kupunguza msongamano na kugusana Amesema Askofu Msonganzila.
Amesema Pia waamini wote kuzingatia Kanuni za usafi ,kwa kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kuingia Kanisani ,katika Sala na adhimisho la Misa,Maji ya Baraka yanayokuwa mlangoni mwa Kanisa ya kujibariki yaondolewe,pamoja na Ekaristi Takatifu kupokelewa katika mikono tu na sio mdomo.

Pia amewataka Mapadri watumie Pamba kuwapaka watu mafuta wakati wa Ubatizo,Kipaimara na mpako wa wagonjwa,Mapadri wasiwaguse waamini wakati wanawabariki,na ameongeza kuwa hakuna kutakiana amani kwa kushikana mikono bali ishara nyingine zitumike kama vile kuinamiana kwa mbali na kupungiana mikono,au kuangaliana na kuonyesha tabasamu.
Askofu Msonganzila amebainisha kuwa ni vema mtu akafunga mdomo na pua wakati wa kupiga chafya au wakati analia na anapokuwa karibu na watu Kanisani au katika mikutano,kujiepusha kuwashika wagonjwa hata wa majumbani bila kinga ya mikononi,na zaidi waamini na wananchi kwa ujumla wazingatie maelekezo yanayotolewa na Wizara ya,Maendeleo ya jamii,jinsia na watoto juu ya namna virusi hivyo vinavyoambukizwa.

Amewaomba waamini kuendelea kuomba Mungu kwa Imani ,uponyaji na uvumilivu kwa ajili ya wenzetu walioathirika na Mwenyezi Mungu atuepushe na janga hilo. “Busara itatulinda,ufahamu utakuhifadhi”(Mit.2:11)