Tuchague Viongozi Wenye Sifa Wasiotoa Rushwa-Ask.Msonganzila

17/04/2024

Askofu wa Jimbo katoliki la Musoma Michael Msonganzila amewakumbusha wakristo nchini kuhakikisha wanapoelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na baadae uchaguzi mkuu, wanachagua kiongozi mwenye sifa na anayeweza kuwatumikia kwa haki na kumwogopa mtu anayetumia hongo kupata madaraka kwa kuwa mtu wa aina hiyo sio mpenda amani na hana hofu ya Mungu.

Askofu Msonganzila ameyasema hayo wakati wa homilia alipokuwa akitoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa waamini 76 wa Parokia ya Mtakatifu Bikira Maria wa Fatima Parokia ya Songe Jimboni humo, ambapo amesema ni vema waamini wakachagua kiongozi anayependa haki na sio kupokea rushwa na kisha wanamchagua mtu asiye na sifa, kufanya hivyo ni sawa na Yuda aliyemsaliti Yesu.

Usikubali kumsaliti Kristo kwa sababu ya umasikini na ufukara wako, hapo ndipo unapopaswa kumshuhudia Kristo na wala tusipokee hela yake wakati tunajua hatutamchagua maana hiyo ni dhambi, bora tusimamie ukweli na tumchague mtu mwenye sifa anayestahili na atakaye tuongoza kuyaacha mabaya na kuyatenda mema kisiasa, kidini na kijamiiamesema Askofu Msonganzila.

Tumchague mtu ambaye ana hofu ya Mungu anayeogopa kudhurumu haki ya mtu katika Nyanja zote na mpenda ukweli atakayetuongoza katika kutenda haki kwa kila mtu bila kununuliwa wala kubagua hali na jinsi ya mtu kwa kuwa ,wengi wanaochaguliwa kwa hongo huwa hawatendi haki.

Askofu huyu amesisitiza zaidi jumuiya zetu kuwa mstali wa mbele katika kudumisha upendo na kuendelea kutetea haki na amani katika jamii zetu ili kuendelea kumtangaza kristo mfufuka kwa matendo mema ambaye ndiye msingi dhabiti wa imani yetu wakristo.

Paroko wa Parokia hiyo Padri Wilbert Matembo amemshukuru Mhashamu Baba Askofu kwa kufanya ziara ya kichungaji katika Parokia hiyo na kuwaimarisha kiimani waamini 76 kwa sakramenti ya Kipaimara, sambamba na kujionea shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanyika katika Parokia hiyo, ambapo amesema ujio wake umewaongezea zaidi nguvu ya kiimani waamini wa Parokia hiyo.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo Filbert Rwiza amewashukuru waamini kwa mapokezi ya ujio wa Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo hilo katika Parokia yao na kusema kuwa hakika wameonja upendo wa Baba kama mchungaji mkuu wa kondoo katika Jimbo hilo.