Wakristo Nchini Ondoeni Vikwazo Muwe Karibu Na Mungu -Padri Duda

15/05/2024

Wakristo nchini wamekumbushwa kuondoa vikwazo vyote vinayosababisha washindwe kuwa karibu na Kristo hasa kwa kutenda matendo mema na kujiepusha na yale yanayomchukiza Mwenyezi Mungu.

Hayo yamebainishwa na Paroko wa Parokia ya Buhemba Padri Mathias Braun Duda katika homilia yake Dominika ya sherehe ya kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, sambamba na kuhitimisha kongamano la kwanza la Vijana Wafanyakazi Wakatoliki (VIWAWA) Dekania ya Butiama ambalo limefanyika kwa siku tatu.

Flowers in Chania

Padri Duda amesema tunatakiwa kufahamu kuwa mwisho wa maisha yetu ni mbinguni hivyo basi yote tunayoyafanya hapa duniani yanapaswa kuwa mambo yanayompendeza na kumtukuza Mungu.

Upungufu wa imani yetu ndiyo unatufanya tuendelee kutenda dhambi ,tunatoa rushwa tunasema uongo,tabia zetu mbaya zitatupeleka wapi,tunawajibu wa kuhubiri neno la Mungu kwa kila kiumbe,tumesahau kuhubiri injili ndani ya familia zetu, Jumuiya na Parokia zetu, injili haihubiriwi tumebaki tunaongea juu juu tu kwa hofu ya kuwa nikiwaambia watu ukweli hawatakuja kanisani,wewe sema ukweli tu hata kama watu wataumia ili utimize wajibu wakoAmesema Padri Duda.

Amesema ili kuwa karibu na Mungu ni vema kuacha chuki,kupunguza ugomvi,kutokutoa rushwa,kujikita katika sala,kuondoa vikwazo vyote ulivyonavyo na zaidi kupata amani ndani ya moyo wako ili kuwa huru mbele ya Kristo.

Mlezi wa vijana hao katika udekano wa Butiama Padri Yohana Kachwele CR amesema vijana wanatakiwa kukumbushwa mara kwa mara umuhimu wa kuwa karibu na Kristo na ndio maana wameandaa kongamano hilo ili kuwajenga zaidi kiroho na kimwili.

Mwenyekiti wa viwawa Jimbo Katoliki la Musoma Phinias Luzangi amewapongeza Dekania ya Butiama kwa maandalizi mazuri ya kongamano hilo sambamba na mada mbalimbali zilizotolewa kwa vijana hao ambao ndio nguzo ya Kanisa.