Mahujaji Tumtangaze Kristo Kupitia Matendo Yetu-Padri Wojciech

26/05/2024

Mahujaji wa chama cha Kitume cha Mtakatifu Rita wa Kashia wameaswa kuishi maisha halisi ya somo wao ili kuhakikisha wanajichotea baraka na neema kupitia Mtakatifu huyu sambamba na kuwa mfano wa kuigwa na waamini wengine ndani na nje ya Kanisa.

Hayo yamesemwa na Mhifadhi Mkuu wa Kituo cha Hija cha Kitaifa cha Huruma ya Mungu Kiabakari na Paroko wa Parokia hiyo Padri Wojciech Adam wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Mtakatifu Rita wa Kashia ambayo hufanyika kila mwaka mei 22.

Kuweni mfano bora katika Kanisa,umoja ,mshikamano mliouonyesha na kufanya maamuzi ya kutembelea vituo vya Hija hasa hapa kwetu Kiabakari na kutembelea kaburi la hayati baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Kawekamo na kwingineko isiwe kutembea kama maonyesho bali mhakikishe mnaendana kimatendo na kiimani zaidi katika kuyatenda yale yaliyotendwa na Mtakatifu somo wenu Amesema Padri Wojciech.

Amesema kuwa ujio wao hapa katika kituo cha hija Kiabakari ni kuonyesha ukomavu katika kumtumikia Kristo na kujisogeza karibu naye,kwani wangeweza kufanya mambo mengine ambayo hayaendani kabisa na siku hiyo.

Mwenyekiti wa Utume huo Angela Kessy kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam amesema lengo kubwa la kufanya hija hiyo ni kujiandaa kiroho lakini pia kumkabidhi Mungu changamoto mbalimbali tunazozipitia kama kanisa na Taifa ili aweze kutusaidia katika kuzitatua.

Amesema katika hija yao watatembelea kaburi la Mwalimu Julius kambarage Nyerere ili kumuomba Mungu mchakato wa Mtumishi wa Mungu kutangazwa kuwa Mtakatifu uweze kukamilika na hatimaye awe Mtakatifu.

Amewakumbusha wakristo wote kuendelea kumuomba Mungu Amani, upendo na mshikamano vidumu milele kwa ajili ya kizazi kijacho.