Vijana Tangazeni Amani,Msitumike Vibaya na Wanasiasa Kipindi cha Uchaguzi

27/06/2024

Vijana Wafanyakazi Wakatoliki (VIWAWA) wameaswa kuacha kutumiwa na wagombea wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu 2025 badala yake wale wenye uwezo wa kuongoza wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali ili kuongeza idadi kubwa ya vijana katika kusukuma maendeleo ya nchi.

Hayo yamesemwa na Padri Benedicto Luzangi wakati wa Kongamano la 5 la Viwawa Jimbo Katoliki la Musoma lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya Tarime iliyopo katika Parokia ya Tarime Jimboni humo,ambapo zaidi ya vijana 200 wameshiriki kongamano hilo.

Padri Luzangi amesema vijana wengi wamekuwa wakitumika vibaya na mara nyingi wamekuwa wakijikuta katika wakati mgumu hasa vurugu zinapotokea na kusababisha wengi wao kuumia na hata kupoteza maisha,hivyo kujikuta nguvu kazi ya kanisa au Taifa inapotea kutokana na wengine kujiingiza katika vurugu ambazo zinahatarisha maisha yao na familia zao.

Tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi karibuni,naomba niwaambie wale wenye kalama za uongozi jitokezeni kugombea, na ninyi vijana waungeni mkono wenzenu wanaokuwa wamejitokeza kugombea nafasi,lakini itakuwa aibu au fedheha kwa kanisa kusikia kuwa kuna vurugu zimetokea sehemu fulani na vijana wamekamatwa wamo ndani harafu tukute ni vijana wetu viwawa itakuwa ni aibu sana,gombeeni nafasi na wala msitumike vibaya.amesema Padri Luzangi.

Mwenyekiti wa Viwawa Jimbo Katoliki la Musoma Phinias Luzangi amesema ni kweli vijana wamekuwa wakitumika katika uchaguzi wa viongozi, lakini kongamano hilo limewakutanisha vijana ili waweze kuelezana mambo muhimu ya kuzingatia katika kuelekeza chaguzi zote ili wasiwe sehemu ya machafuko wakati wa uchaguzi bali wawe nuru katika kudumisha amani ya Taifa letu.

Phinias amewaomba vijana kuendelea kushikamana katika kulitumikia Kanisa kwani vijana ndio nguzo ya kanisa, hivyo ni vema wakaendelea kuwa pamoja kwa ajili ya kazi ya Mungu na Taifa kwa ujumla ili kuendeleza uhai wa Kanisa.

Kwa upande wao vijana walioshiriki kongamano hilo wameushukuru uongozi wa Viwawa Jimbo kwa kuandaa kongamano hilo ambalo huwakutanisha vijana kutoka Parokia zote za Jimbo na kufahamiana zaidi.