Askofu msonganzila akemea vitendo vya ulawiti na ubakaji kwa watoto

04/07/2024

Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila amekemea vitendo vya ulawiti na ubakaji vinavyoendelea hapa nchini ambapo amewataka wazazi/walezi kuongeza ulinzi kwa watoto ili kuwalinda na vitendo hivyo.

Hayo ameyasema wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya kufunga jubilei ya miaka 50 ya jumuiya ndogondogo kijimbo, Misa hiyo imefanyika katika Kanisa kuu la Maria Mama wa Mungu Musoma mjini Juni 29,2024.

Hali ni mbaya kwa watoto sio wakike wala wa kiume ,wazazi jitahidini sana kuwa karibu na watoto hawa ndioTaifa la kesho tusipoongeza ulinzi kwa watoto hawa tutajenga Taifa lenye kizazi cha hovyo kabisa hapo baadae ni vema kila mmoja kupitia mkusanyiko wetu wa kukutana kwenye jumuiya basi tushirikishane zaidi juu ya ulinzi kwa kizazi kijachoamesema Askofu Msonganzila.

Amewaomba waamini kuendelea kuilinda imani yetu kwa kujengeana misingi dhabiti tunayofundishwa kupitia mafundisho yetu ya kanisa na kuhakikisha tunayaishi na hivyo kuwa mfano bora ndani ya familia na katika jamii yetu.

Katika hatua nyingine Askofu Msonganzila amewaomba wananchi kuendelea kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huu wa Serikali za mitaa bila kuvuruga amani ya nchi yetu ili kupata viongozi watakaoongoza.

Askofu huyo amekemea vitendo vya rushwa huku akiwaomba wananchi kutokukubali kuuza haki yao kwani kununuliwa au kuuza haki yao ni kinyume kabisa na maadili na tamaduni za kitanzania.