Mapadri pazeni sauti juu ya vitendo vya ukatili vinavyofanyika katika jamii


Mapadri nchini wametakiwa kuisaidia jamii kupaza sauti juu ya vitendo mbalimbali vya ukatili vinavyoendelea katika jamii.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya siku nne ya kuwajengea uwezo juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia ,iliyoandaliwa na Jimbo hilo ,Mhashamu Baba Askofu wa Jimbo hilo Michael Msonganzila amesema, mapadri wana kila sababu ya kufahamu mambo mbalimbali yanayoashirilia vitendo vya ukatili katika jamii.

"Sisi Mapadri tuna nafasi pia ya kupaza sauti juu ya mambo hayo na sio kuiachia serikali au wanaharakati ,haipendezi tunapomaliza Misa Takatifu tunaishia tu nendeni na Amani bila kuwaambia waamini wetu juu ya ukatili ambao unafanyika katika nyumba zetu,Jimbo katoliki la Musoma na Mkoa wa Mara bado kuna changamoto kubwa ni lazima tuungane kukemea"amesema Mhashamu Baba Askofu Msonganzila.

Mwezeshaji wa semina hiyo kutoka kituo cha Temination Female Genital Multilation (TFGM) Masanga Valerian Mgani amesema kuna haja ya kumsaidia mtoto kwa kutumia mbinu ya ubunifu tofauti na iliyozoleka ili kumuokoa kutoka katika hali ya vitendo vya ukatili hasa ubakaji na ulawiti vinazidi kushika kasi kuzidi hata ukeketaji.

"Mapadri mna nafasi kubwa sana ya kubadilisha jamii kuondokana na hili,kupitia ukatili wa kijinsia kuna haki nyingi zimedidimizwa , kuna vitu vingi sana tunahitaji kuvifanyia kazi ili kuisaidia jamii hasa kundi kubwa linaloongoza kiadhilika likiwa ni akina mama na watoto wa kike"amesema Mgani.

Amesema kuwa sheria za nchi zina ulegevu mkubwa kiasi kwamba faini ya mtoto anayekeketwa faini yake ni ndogo sana milioni mbili,wakati nghariba anapokamatwa ana uhakika wa kupata milioni 10 kiasi ambacho anapolipa milioni 2 bado ana pata faida ya milioni 8.

Kwa upande wao mapadri wa Jimbo hilo wamelipongeza Kanisa kwa kuandaa semina hiyo,ukizingatia kuwa Mkoa wa Mara na Jimbo katoliki kwa ujumla bado linakabiliwa na changamoto kubwa ya vitendo vya ukatili.