CORONA: Askofu Msonganzila awaasa waamini kuchukua tahadahari.

03 / 02/2021

Waamini wa Jimbo Katoliki la Musoma wameombwa kuendela kujilinda na kuchukua tahadhali ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Corona,kutokana na nguvu kali iliyonayo, lakini pia kulingana na hali halisi ilivyo kwa sasa ambayo sio nzuri katika jamii japokuwa serikali haijakanusha kuwepo au kutokuwepo kwa ugonjwa huo.

Akizungumza wakati wa Misa Takatifu ya mshikamano ambayo imefanyika Februari 3 mwaka huu,katika Kanisa la Bikira Maria Mama wa Mungu ,Askofu wa Jimbo hilo Michael Msonganzila amesema licha ya aina mbalimbali zilizokwisha tolewa za jinsi ya kujikinga na corona amewaomba pia watu kutumia kuvuta mvuke wa maji yaliyochemka sana ,na kisha kutoa mvuke huo kwa kutumia mdomo ili kujinusuru na hali ya maambukizi kulingana na mazingira yao.

“Corona yupo tuliyempata mwanzoni alikuwa Covid 19 huyu sasa ni Covid 21 ana nguvu kali kuliko ile ya 2019,serikali inasisitiza sana tuchukue tahadhali ikiwa ni pamoja na kupiga nyungu,kupata sanitizer ,na kunawa mikono ,kubwa zaidi ni kwamba tusisahau unywa maji moto walau mara tano kwa siku itasaidia sana”amesema Askofu Msonganzila

Askofu Msonganzila amewaomba mapadri kuendelea kuwakumbusha waamini makanisani kuhusu namna ya ukaaji kwenye mabenchi kwa kuzingatia mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine,sambamba na kunyoosha mkono wakati wa kupokea ekaristi Takatifu wakati wa komunyo ili kuweka umbali.

Akisisitiza kuhusu chanjo zinazoendelea kutolewa kwa ajili ya kujikinga amesema hakuna udhibitisho uliokwisha tolewa juu ya chanjo hizo ,maana hata waliokwisha chanjwa wamewahi kuanguka hivyo, yatupasa kuchukua tahadhali kwa ajili ya manufaa yetu na Taifa letu kwa ujumla.

Amewaomba wazazi na walezi kuona namna ya kuwasaidia kujikinga kwani wanapotumia kuvuta mvuke wa maji moto lazima kuwepo na uangalizi wa kutosha ili wasiungue,wakaleta madhara mengine kwenye ngozi na hivyo kusababisha matatizo makubwa.