Kamati ya Bunge Yaridhishwa na Mazingira Mazuri ya Chuo Cha Ufundi St. Anthony Musoma

20/03/2024

Flowers in Chania

Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma za maedeleo na Ustawi wa Jamii iliyoongozana na Waziri wa Kazi na Ajira Profesa Joyce Ndalichako, imeridhishwa na vifaa vilivyopo vya kufundishia wanagenzi pamoja na miundombinu ya Chuo cha Ufundi cha Mt. Anthony kilichopo Parokia ya Nyamiongo Jimbo Katoliki la Musoma, walipotembelea chuo hicho.

Wajumbe wa kamati hiyo wamesema wamefurahishwa na mazingira mazuri ya Chuo hicho ambayo ni tofauti na vyuo vingine walivyovitembelea ambavyo wamekuta hali ya vifaa vya kufundishia wanagenzi havipo na wala miundombinu iliyopo haiendanani na uhalisia wa chuo licha ya Serikali kuwekeza kwenye vyuo hivyo.

Uongozi wa chuo hiki umejipanga vizuri kila kitu kimepangwa katika viwango vinavyotakiwa na Serikali ,mheshimiwa Waziri naomba katika bajeti ya Wizara yako uangalie namna gani utaweza kupata fedha za kuwasaidia vijana hawa watakapomaliza basi Serikali iwawezeshe vifaa ,lakini pia wawezeshwe mikopo ile ya vijana iwasaidie kujikwamua kiuchumiamesema Mwenyekiti wa Kamati hiyo Fatma Toufiq

.

Flowers in Chania

Mwenyekiti huyo amesema serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia imejipanga kuwakwamua vijana waweze kuondokana na umasikini, ndio maana kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeweza kuwawezesha vijana wengi kujifunza fani mbalimbali zitakazowawezesha kujiajiri wenyewe na hata kuajiri watu wengine. ameahidi kuongeza vijana wengine zaidi kujiunga na vyuo mbalimbali vya ufundi hapa nchini.

Waziri wa Kazi na Ajira Profesa Joyce Ndalichako amesema Masomo haya wanayoyasoma vijana wanaofadhiliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu yatawasaidia kujiajiri ndani na nje ya nchi kwa kuwa mtaala wake umezingatia viwango vya elimu vya Kimataifa hivyo,wanagenzi hao wasiwe na shaka juu ya wapi watapata ajira bali wawe huru kujiajiri ndani na nje ya nchi.

Naibu Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma na Mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho Padri Julius Ogolla ameishukuru kamati hiyo ya bunge kwa kufika kujionea wenyewe hali halisi ya miundombinu ya chuo hicho pamoja na vifaa vya kujifunzia wanagenzi hao wanaofadhiliwa na Serikali .

Padri Ogolla ameishukuru Serikali ya awamu ya sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukichagua chuo hicho kuwa miongoni mwa vyuo vilivyoteuliwa kupokea wanagenzi wanaofadhiliwa na ASerikali ya awamu ya sita kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu,ambapo ameiomba serikali kuendelea kukiamini chuo hicho na kuleta wanagenzi wengine wengi tena.

Awali akisoma taarifa ya chuo Mtaaluma wa chuo hicho madam Petronila Shirima ameishukuru kamati kwa kufika na kuongea na wanagenzi hao uso kwa uso, sambamba na kuwaomba waendelee kuwasaidia vijana wengine zaidi kwani bado uhitaji ni mkubwa ukizingatia idadi ya wanafunzi 100 wanaofadhiliwa na Ofisi hiyo.

Iddy Kambi mmoja wa wanagenzi hao ameishukuru Kamati kwa kufika kuwaona namna wanavyojifunza na zaidi amewaomba wafikishe salam za shukurani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuwafadhili vijana hao ambao walikuwa mtaani hawana fani yoyote ili wajikwamue na umasikini wa fikra lakini pia wa kipato kwani kwa sasa wana uhakika kuwa mara baada ya kuhitimu masomo yao watakuwa na uwezo wa kujipatia kipato wenyewe na kuondokana na utegemezi katika familia zao.