Tukatae Rushwa Haki Itendeke-Padre Ogolla

03/04/2024

Wakristo walio na nafasi katika ofisi za Umma wamekumbushwa kuwa waaminifu na kujiepusha na matendo yanayomnyima mtu haki yake ,hasa kwa kupokea rushwa ambayo imekuwa chanzo cha haki kupokonywa na wenye fedha katika jamii. .

Hayo yamesemwa na Naibu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Padri Julius Ogolla wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Pasaka katika Parokia ya Mtakatifu Agostino Mwisenge, Jimboni humo.

Padri Ogolla amesema katika ulimwengu wa sasa kumekuwepo na dhuruma nyingi sana kwa watu wasio na makosa hali inayochangia vitendo vya rushwa viendelee kuwepo kwa madai kuwa usipotoa rushwa huwezi kutendewa vyema.

Rushwa ina gharama yake,ukipindisha haki leo iko siku ukweli utawekwa wazi,tujifunze kutoka kwa Yuda aliyemsaliti Yesu kwa vipande 30 vya fedha lakini mwisho wa siku Yesu alisulubiwa na akafa Msalabani siku ya tatu alifufuka mzima, ndio maana leo tunasherehekea ushindi na hata aliyemsaliti aliona aibu,kumbe tusiwatendee watu mabayaamesema Padri Ogolla .

Amewakumbusha pia kuendelea kuwasaidia wahitaji kwani wengi wamekuwa na desturi ya kuwasaidia wahitaji kipindi cha kwaresma tu na baada ya Pasaka hawawakumbuki tena,moyo tuliokuwa nao kipindi cha kwaresma uendelee hivyo hivyo hata baada ya Pasaka.

Vedastus Masige muumini wa Parokia hiyo amewaomba waamini wote wanaopitia changamoto za maisha kuendelea kusali na kutokata tamaa kwani Bwana wetu Yesu Kristo alishinda kifo na mauti kwa kuwa aliyavumilia yote yaliyompasa kuyapitia,hivyo ni vema tukamtazama yeye na kumkabidhi maisha yetu yote.

Ester John amewapongeza waamini wote kwa kufikia siku ya leo kwa kuwa sio wote waliotamani kuifikia siku ya Pasaka na wamefika, wengine wameshindwa kutokana na changamoto mbalimbali za maisha ikiwemo kifo magonjwa na hata umasikini na kuwaomba waendelee kuombeana na kuliombea Taifa letu Amani ya kudumu.